Mwanaume mmoja kipofu wa nchini Uingereza ameweza kumuona mkewe kwa mara ya kwanza baada ya kufanyiwa upasuaji wa macho ambapo jino lake la juu lilipandikizwa kwenye jicho lake. Mjenzi Martin Jones, 42, alipata upofu wa macho yake yote mawili zaidi ya miaka 10 iliyopita baada ya bomba la madini ya aluminium yaliyokuwa yamechemka kumpasukia usoni, liliripoti gazeti la Daily Mail la Uingereza.

Lakini sasa baada ya kufanyiwa upasuaji wa macho wa aina yake ambapo jino lake lilipandikizwa kwenye jicho lake la kulia, ameweza kuona kwa mara ya kwanza baada miaka mingi sana ya upofu.

Upasuji kama huu umefanyika mara 50 tu nchini Uingereza.

Upasuaji huo wa macho umemwezesha Jones aweze kumuona kwa mara ya kwanza mkewe Gill ambaye alimuoa miaka minne iliyopita wakati akiwa tayari ni kipofu.

"Madaktari waliitoa bandeji kwenye jicho langu na mara nikaanza kuona kitu mbele yangu na nilipoangalia vizuri alikuwa ni yeye mke wangu".

"Ni mrembo sana , sikuwahi kumuona awali, ilikuwa ni miujiza kumuona kwa mara ya kwanza" alisema Martin.

"Wakati nilipoona kuna uwezekano wa kuona kwa mara nyingine, mtu wa kwanza niliyetaka kumuona alikuwa ni mke wangu".

Opereshereni hiyo ya masaa manane iligunduliwa na daktari mwenye makazi yake nchini Uingereza, Dr Christopher Liu.

Upasuaji ulifanyika kwa kuchukua jino lake moja la juu la mbele kwa pembeni na jino hilo lilitengenezwa katika umbile ambalo liliweza kuwa kama nyumba ya lenzi moja ndogo iliyotengenezwa maalumu.

Jino lake lilitumika kwa kuwa mwili wa binadamu mara nyingi hukataa kuendana na plastiki, alisema Dr Liu.

Kipande cha ngozi yake kilichukuliwa kutoka kwenye ngozi ya mashavu yake na kupandikizwa kwenye jicho lake kwa muda wa takribani miezi miwili na kiliweza kupata uwezo wa kujisambazia damu chenyewe.

Baadae kipande hicho kilitolewa na kuwekwa juu ya jino lake ambalo liliwekwa lenzi na kupandikizwa ndani ya jicho lake na kitobo kidogo kilitobolewa kwenye ngozi hiyo iliyowekwa juu ya jino ili kuwezesha mwanga kuingia na kumwezesha Martin kuona tena.

Madaktari walisema kwamba upasuaji kama huu hufanyika kwa watu wenye upofu uliosababishwa na kuharibika kwa cornea na ambao macho yao hayawezi kufanyiwa upasuaji wa aina zingine wa upandikizaji wa cornea.

[ Cornea ni eneo la juu la jicho ambalo linazunguka iris, pupil na anterior chamber. ]

Martin hakufanyiwa upasuaji kama huu kwenye jicho lake la kushoto kwakuwa jicho hilo lilikuwa limeharibika sana na ilibidi litolewe.