Familia moja nchini Marekani inahaha kutafuta tiba ya ugonjwa usiojulikana ambao umemfanya mtoto wao wa miezi 10 kuzidi kuwa mdogo badala ya kukua. VIDEO ya mtoto huyo mwisho wa habari hii. Michelle na mumewe Sean Agnew wakazi wa Utah nchini Marekani wanahaha kutafuta tiba ambayo hadi leo haijapatikana ya mtoto wao Maggie ambaye badala ya kukua kama watoto wengine amezidi kudhoofika na kuwa mdogo.

Maggie mwenye umri wa miezi 10 hivi sasa anazidi kuwa mdogo kwani misuli kwenye mwili yake inayeyuka na kumwacha na nyama zinazoning'inia, anapoteza kilo kila siku pamoja na kulishwa chakula kingi sana.

Hadi sasa madaktari hawajajua nini kinamsumbua mtoto huyo kwani uzito wake umezidi kupungua na misuli kwenye mwili wake imezidi kunywea pamoja na kwamba madaktari waliamua walimshe kwa kutumia mipira iliyounganishwa kwenye tumbo lake ambayo husukuma kalori nyingi kuliko kawaida.

"Anapata kalori nyingi sana kutoka kwenye chakula anacholishwa lakini mwili wake hutumia kalori zote katika muda mfupi , hali ambayo imetufanya tusielewe chakula anacholishwa huwa kinaenda wapi" alisema baba wa mtoto huyo.

Vipimo vya magonjwa yote ambayo madaktari walihisi yanaweza yakawa ndio chanzo cha hali hiyo yamefanyika lakini vipimo vyote havijathibitisha ugonjwa wowote ule.